TBD
Mjadala wa BK juu ya uchunguzi wa mashambulio ya Tarafa ya Ghaza waingia siku ya pili
Ijumatano Baraza Kuu (BK) la UM lilianzisha majadiliano maalumu kuhusu ripoti ya uchunguzi wa UM, uliofichua vikosi vya Israel pamoja na wapiganaji wa KiFalastina, walipatikana na hatia ya kukiuka haki za kibinadamu wakati wa mashambulio ya katika eneo liliokaliwa la Tarafa ya Ghaza mapema mwaka huu.
Ripoti inayojulikana kama Ripoti ya Goldstone, ilijumlisha matokeo ya uchunguzi wa miezi mitatu, ulioongozwa na Jaji Richard Goldstone wa Afrika Kusini, aliyekuwa mwendesha mashitaka wa mahakama ya UM juu ya makosa ya vita kwa iliokuwa Yugoslavia, uchunguzi ambao vile vile uliidhinishwa na Baraza la UM juu ya Haki za Binadamu. Tume ya uchunguzi ilijumlisha wataalamu wanne wa kimataifa, na iligundua ushahidi uliothibitisha kihakika kwamba makundi husika na mikwaruzano iliotukia kati ya mwezi Disemba 2008 mpaka Januari 2009, katika Tarafa ya Ghaza, walikiuka sheria za kimataifa za kiutu kuhusu usalama na hifadhi ya raia kwenye mazingira ya mapigano, hali ambayo ilijumuisha makosa makuu ya jinai dhidi ya binadamu. Kadhalika, Baraza Kuu, ambalo leo limeingia siku ya pili ya majadiliano, linazingatia mswada wa azimio liliowasilishwa na wanachama wa Jumuiya ya Mataifa Yasiofungamana na Sera za Mataifa Makuu (NAM) na Kundi la Mataifa Wanachama wa Nchi za KiArabu, ambayo yameunga mkono matokeo ya Ripoti ya Tume ya Uchunguzi ya UM, na wakati huo huo kumtaka KM atume ripoti hiyo kwa Baraza la Usalama kuzingatiwa na kuamuliwa. Baraza Kuu linatarajiwa kupitisha azimio juu ya Ripoti ya Uchunguzi kuhusu Mashambulio ya Tarafa ya Ghaza baada ya majadiliano kukamilishwa alasiri Alkhamisi.

