TBD
UM umeanzisha mradi mkuu wa kusambaza vifaa vya kusajili wapiga kura Sudan
Shirika la UM juu ya Ulinzi Amani Sudan Kusini (UNMIS) na Shirika la UM juu ya Miradi ya Maendeleo (UNDP) yameanzisha operesheni kuu, za kugawa vifaa vya uchaguzi vitakavyotumiwa kusajilia wapiga kura kuanzia Ijumatatu ya leo.
Wapiga kura hawa wanatazamiwa kushiriki kwenye uchaguzi wa vyama vyingi utakaofanyika Sudan mwaka ujao. Vifaa vya kuhudumia uchaguzi, vyenye uzito wa kilo 120,000 (laki moja na elfu ishirini), ikijumlisha vifaa vya kusajilia wapiga kura, fomu za uchaguzi na vifaa vya mafunzo ya maandalizi ya uchaguzi, vile vile, vitapelekwa kwenye maeneo yaliotambuliwa rasmi na Kamisheni ya Uchaguzi ya Taifa (NEC) kutumiwa katika upigaji kura. Shirika la UNDP limefadhilia gharama ya kusafirisha vifaa hivyo kwenye miji 25 ya majimbo ya Sudan. Vile vile watumishi wa UNMIS wanasaidia kuvisafirisha vifaa vya uchaguzi wakati maofisa wa Kamisheni wanasimamia utekelezaji wa taratibu na kanuni za usajili wa wapiga kura katika darzeni ya maeneo yenye matatizo kuyafikia, na yale yalio mbali, hasa katika Sudan Kusini na Kordofan Kusini. Kadhalika, Vikosi vya Mchanganyiko vya UM-UA kwa Darfur (UNAMID) vinasaidia kupeleka vifaa vya uchaguzi kwenye maeneo ziada yaliojitenga yaliopo Darfur Magharibi na Darfur Kaskazini. Kamisheni ya NEC imeiomba UNMIS, kusimamia huduma za kiufundi zinazohitajika kuendesha uchaguzi wa vyama vyingi katika Sudan mwaka ujao, kwa utaratibu wenye kuaminika, na ulio wazi.

