TBD
Mfuko wa CERF kuifadhilia IOM msaada wa kuhudumia makazi ya muda wahamiaji wa Usomali
Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) limeripoti kuwa litapokea msaada wa dola milioni 2.6 kutoka Taasisi ya Mfuko wa UM juu ya Maafa ya Dharura au Mfuko wa CERF, fedha zitakazotumiwa kuwasaidia kupata makazi ya dharura wahamiaji 12,700 wa Usomali ambao wanabanana hivi sasa kwenye kambi za Kakuma, ziliopo Dadaab, kwenye jimbo la kaskazini-mashariki ya Kenya.
Operesheni hii ya uhamisho itachukua miezi mitatu kukamilishwa na itajumuisha huduma za UNHCR, Idara ya Masuala ya Wahamiaji ya Kenya na mashirika yasio ya kiserikali. Safari ya uhamisho itachukua kilomita 1,200, na kabla ya hapo wahamiaji watapimwa afya kuona kama wana uwezo wa kusafiri safari ndefu kama hiyo. Wahudumia afya vile vile wanatarajiwa kusafiri na wahamiaji. Wahamiaji walio na umri mrefu, walio wagonjwa na wanawake wajawazito wanatarajiwa kuhamishwa kwa ndege.

