TBD
Idadi kubwa ya wahamaji wa Usomali na Ethopia wanaotoroshwa Afrika Kusini huteswa na wafanya magendo, inaripoti IOM
Shirika la Kimataifa juu ya Wahamaji (IOM) limetoa ripoti mpya kuhusu "uhamaji usio wa kawaida" ambao huwatesa wale watu wanaotoroshwa kimagendo kutoka Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika, wanaopelekwa Afrika Kusini.
Ripoti ilibainisha idadi kubwa ya wahamiaji hawa hughilibiwa na wafanya magendo, kila siku, wahalifu ambao huwatesa na kuwakandamiza, na pia kuwafedhehesha, kuanzia muda wahamiaji wanapoondoka makwao mpaka pale wanapowasili Afrika Kusini. Wakifika huko, kwa mujibu wa ripoti, baadhi ya wahamiaji huamua kuendelea na safari na kuelekea mataifa ya Ulaya, Marekani au Australia kutafuta maisha. Mada ya ripoti ina kaulimbiu isemayo "Waathirika wa Haja za Lazima Kimaisha: Wafukuzia Ndoto ya Kusini". Ripoti ilitayarishwa kufuatia mahojiano na watu 800, waliojumlisha wahamiaji wenyewe, wawakilishi wa jamii kadha wa kadha za, maofisa wa kitaifa pamoja na wajumbe wa jumuiya za kiraia na pia wale wa kutoka sekta ya binafsi, na vile vile kujumuisha wahojiwa waliopo katika mataifa wanayopita njia, na kwenye nchi wanazomalizia safari zao, yakiwemo mataifa ya Ethiopia, Kenya, Malawi, Msumbiji, Jamhuri ya Afrika Kusini, Tanzania na Zambia. Matokeo ya utafiti yalibainisha wahamiaji wa kiume wanaotoroshwa huteswa, kikawaida, na wafanya magendo pamoja na majambazi wa kienyeji - na mara nyengine huteswa hata na maofisa wa serikali ambao hutarajiwa kuupatia umma huo kinga na hifadhi inayolinagana na kanuni za kimataifa, badala ya kuwatesa. Ripoti ilidhihirisha baadhi ya maofisa wa serikali huwanyanyasa wahamaji, huwapiga na kuwaibia amana zao, na mara nyengine hata huwanajisi kimabavu, mambo ambayo yanatengua kihakika hyaki za binadamu. Kinyume na Itifaki ya Usafirishaji wa Magendo, inayozingatia kuharimisha vitendo vya kufanya magendo na kuwapatia hifadhi wahamaji wanaotoroshwa, nchi kadha bado zinaendelea kuwaweka vizuizini na kuwatia hatiani wahamaji badala ya wafanya magendo, wahalifu ambao wanaendelea kustarehea makosa ya jinai bila kukhofu kuadhibiwa. Ilibainishwa na ripoti ya kuwa wahamiaji wa kiume 20,000 ziada kutoka Ethiopia na Usomali hutoroshwa kila mwaka kutoka Pembe ya Afrika na kupelekwa Jamhuri ya Afrika Kusini, baada ya kulipa, kwa wastani, dola 2,000, malipo ambayo huongezeka zaidi ikiwa wahamiaji husafiri kwa ndege kwenda Afrika Kusini katika baadhi ya safari. Ripoti ya IOM ilisema idadi kubwa ya wahamaji hawa husafirishwa kimagendo kwa kutumia barabara, na mara nyengine hutumia bahari, hususan wale wahamaji wa Kisomali, ambao husafiri kwenye vijimashua vibovu kutokea mji mkuu wa Mogadishu, au kutokea bandari ya kusini ya Kismayo mpaka Mombasa (Kenya), Dar Es Salaam (Tanzania), au Mocimboa (Msumbiji) na kuelekea Afrika Kusini.

