Ban alihutubia Baraza Kuu baada ya kuhitimisha ziara yake Sahel

Kusikiliza /

Katibu Mkuu, Ban Ki-moon

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, amelihutubia Baraza Kuu leo Jumatatu, baada ya kuhitimisha ziara yake kwenye ukanda wa Sahel, hotuba hiyo ikianza kwa kutoa risala za rambi rambi na pole kwa serikali na watu wa Ufilipino kufuatia janga la kimbunga Haiyan.

Kuhusu eneo la Sahel, Bwana Ban amesema ujumbe wake yeye na viongozi wengine kwenye ziara hiyo, akiwemo rais wa Benki ya Dunia, Jim Yong Kim, rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, Donald Kaberuka, na Mwakilishi wake maalum kwenye eneo hilo, Romano Prodi, ulikuwa ni usalama na maendeleo ni lazima viende sambamba.

"Kimoja kinategemea kingine. Viongozi wote tulokutana nao wakati wa ziara yetu, walitambua hili, na kukubali mkakati wetu wa pamoja wa Umoja wa Mataifa kuhusu eneo la Sahel, kama jukwa la kuchukua hatua."

Bwana Ban amelihutubia Baraza hilo pia kuhusu masuala mseto, yakiwemo hali nchini Syria, ambalo amelitaja kuwa tishio kubwa zaidi duniani kwa amani na usalama wa kimataifa. Amsemea Umoja wa Mataifa unaendeleza juhudi zake kwenye nyanja tatu, zikiwemo kuhakiki na kuteketeza silaha za kemikali, kutoa misaada ya kibinadamu ya kunusuru maisha na kutafuta suluhu la kisiasa.

Jingine limekuwa ni kuhusu habari nzuri kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo,  DRC, kufuatia waasi wa M23 kutangaza kukomesha uasi wao wa kijeshi, na serikali ya DRC kudhibiti tena maeneo yote yalokuwa ngome za M23. Bwana ban amesema ni muhimu kwa serikali kurejesha utawala wake kwenye eneo la mashariki mwa DRC, na kuhakikisha watu wa eneo hilo wanafurahia amani.

"Ufanisi wa kijeshi utahitajika kuendelezwa kupitia kukabiliana na vyanzo vya migogoro katika nchi hiyo.  Tukumbuke kuwa bado kuna makundi mengine yenye silaha yanayoendelea kuihangaisha mashariki ya DRC. Kusaini makubaliano ya ushirikiano amani na usalama mapema mwaka huu, kulitoa nafasi ya kipekee kwa DRC na ukanda mzima"

Bwana Ban amegusia pia suala la Jamhuri ya Afrika ya Kati, akisema kuwa mzozo wa CAR unapaswa kutatuliwa kwa njia ya kina kwa kuchukua hatua za dharura na za dhati, huku masuala yote ya kiusalama, kisiasa, haki za binadamu na hali ya kibinadamu vikizingatiwa.

Mengine alozungumzia ni suala la nyuklia Iran na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Watu wa Korea, mabadiliko ya tabianchi, na ajenda ya maendeleo baada ya 2015.

Kipindi Kamili
Kipindi Kamili
Loading the player ...

 

Disemba 2017
T N T K J M P
« nov    
 123
45678910
11121314151617
18192021222324
25262728293031