Uharibifu wa mtambo wa silaha za kemikali Syria wakamilika: UM-OPCW

Kusikiliza /

Wakaguzi, OPCW

Ujumbe wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na shirika la kimataifa la kupinga matumizi ya silaha za kemikali, OPCW umethibitisha kuwa serikali ya Syria imekamilisha uharibifu wa mtambo muhimu wa kutengeneza silaha za kemikali. Ripoti ya Assumpta Massoi inafafanua zaidi.

(Taarifa ya Assumpta)

Taarifa iliyotolewa leo imekariri ujumbe huo ukisema kuwa mtambo huo unahusiana na maeneo yote ya uzalishaji wa silaha za kemikali yaliyokuwa yamewekwa bayana na Syria na hivyo kwa kuharibiwa mtambo huo, haiwezi kufanya kazi tena.

Wamesema kwa mantiki hiyo Syria imekidhi muda uliokuwa umetolewa wa hadi tarehe Mosi Novemba iwe imekamilisha kazi. Ujumbe huo wa watu wanane umerejea The Hague, Uholanzi na kulakiwa na Mkurugenzi Mkuu wa OPCW Ahmet Üzümcü.

Amesifu ujasiri wa ujumbe huo uliokuwepo Syria tangu tarehe Mosi Oktoba na kuweza kukagua maeneo 21 kati ya 23, ambapo hayo mawili hayakuweza kukaguliwa kutokana na sababu za kiusalama, lakini serikali ya Syria ilithibitisha kuwa ni maeneo yaliyotelekezwa siku nyingi na vifaa vyake kuhamishiwa maeneo mengine ambayo yalishakaguliwa.

Katika hatua nyingine Khawla Mattar ambaye ni msemaji wa mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa nchi za kiarabu nchini Syria, Lakhdar Brahimi amezungumzia hatua ya mazungumzo anayoendelea kufanya mjumbe huyo huko Damascus.

(Sauti ya Khawla)

"Bwana Brahimi amekutana na Rais Bashar Al Assad na Waziri wa Mambo ya Nje na wamethibitisha utayari wa kushiriki mkutano wa pili wa Geneva bila masharti yoyote. Brahimi pia amekutana na wawakilishi wa vikundi vya upinzani na makundi ya wanawake na kiraia na wengi wao wamesema wako tayari kushiriki mkutano wa Geneva na wanaunga mkono hatua zote pamoja na suluhu la kisiasa kwenye mzozo huo."

Kuhusu tarehe ya mkutano huo, Bi. Khawla amesema tarehe ya mkutano wa Geneva itatangazwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon na hata mialiko itatolewa na ofisi yake lakini jambo kubwa ni pande kuu husika yaani serikali ya Syria na upinzani ziwe tayari.

 

Kipindi Kamili
Kipindi Kamili
Loading the player ...

 

Aprili 2017
T N T K J M P
« mac    
 12
3456789
10111213141516
17181920212223
24252627282930