Kamishna Guterres ahofia idadi kubwa ya wakimbizi wanaoingia Kaskazini Mashariki mwa Sudan ya Kusini
Kusikiliza /Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, ameelezea hofu yake kuhusu kuzorota kwa hali ya kibinadamu katika jimbo la Upper Nile la Sudan ya Kusini, ambako shirika hilo la UNHCR na wadau wengine wa kutoa huduma za kibinadamu, wanakabiliana na ongezeko la ghafla la idadi ya wakimbizi wanaowasili kutoka jimbo la Blue Nile la Sudan.
Katika kipindi cha wiki tatu zilizopita, takriban wakimbizi 35,000 wamewasili katika jimbo la Upper Nile, ambalo tayari lina wakimbizi 70,000. Wengine wengi wanaendelea kuwasili.
Bwana Guterres ameelezea kusikitishwa kwake na hali waliyomo wakimbizi hao, ambao hawana maji ya kunywa, na wengine wamebaki kula majani ya miti.
Shirika la UNHCR linaamini kuwa wengi wa wakimbizi katika jimbo la Upper Nile wapo karibu sana na mpaka, na hivyo linahofia usalama wao. Usafirishaji wa wakimbizi hawa hadi maeneo salama ni mgumu, kwani wanatumia malori na trekta, na barabara ni mbovu kwa sababu ya mvua ya hivi karibuni.
